Zuchu ateuliwa kuwania tuzo za Burudani Afrika huko Marekani.

Kitinda mimba wa sasa wa WCB yaani Wasafi kampuni ya muziki inayomilikiwa na Diamond Platinumz ameshapata uteuzi wake wa kwanza kuwania tuzo za kimataifa ilhali amejitosa ulingoni mwaka huu tu.

Zuchu kwa jina halisi Zuhura Kopa ameteuliwa kuwania tuzo katika kitengo cha msanii mpya bora yaani ‘Best New Artist’ katika tuzo hizo zinazojulikana kama “African Entertainment Awards USA”.

Anaoshindana nao ni Masauti wa Kenya, Daddy Andre na John Blaq wa Uganda na Olakira wa Nigeria kati ya wengine.

Masauti, msanii wa Kenya

Bosi wake Diamond ameteuliwa katika kitengo cha mtumbuizaji bora na anashindana na Rayvanny na Harmonize wa Tanzania, Yemi Alade, Tiwa Savage, Burna Boy na Wizkid wa Nigeria, Innos B wa Congo, Eddy Kenzo wa Uganda na Jah Prayzah wa Zimbabwe.

Tuzo za “AEAUSA” zilianzishwa mwaka 2015 kwa lengo la kutambua ufanisi wa Afrika katika nyanja mbali mbali hasa burudani, ujasiriamali na uongozi.

Tuzo zaidi ya 30 hutolewa kila mwaka kwa hafla ya siku katika jimbo la New Jersey Marekani. Hafla ya mwaka huu wa 2020 itaandaliwa tarehe 12 mwezi Disemba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *