Categories
Michezo

Zoo FC yaelekea mahakamani kupinga mkataba wa FKF na Star Times

Kilabu ya Zoo Fc imewasilisha kesi ya dharura katika mahakama ya kutatua migogoro michezoni SDT  kutaka iruhusiwe kucheza mechi zake ligi kuu ya Fkf ,bila kupeperushwa kupitia runinga ya Star Times  baada ya kudinda kusaini mkataba huo .

Zoo fc yenye makao yake katika kaunti ya Kericho imesusia kucheza mechi zake mbili za ufunguzi za ligi kuu kutokana na kutokubaliana na mkataba huo, huku ikijiunga na timu za Ulinzi Stars,Mathare United na Gor Mahia ambazo zimesusia kusaini  pia mkataba huo wakidai una vipengee vyenye utata.

Mwenyekiti wa Zoo fc Ken Ochieng’ amemtaka Rais wa FKF kukomesha vitisho na kuonyesha mfano mwema wa uongozi akisema hawako tayari kuachilia haki zao za runinga kwa shirikisho.

“Vitisho na unyanyasi havina nafasi  haswa wakati wa swala linalohusu haki za matangazo ya runinga kwa kilabu ,tumeambiwa tupeane haki zetu kwa miaka saba huku tukilipwa  kiwango cha chini cha pesa na hakuna kipengee cha kujiondoa ukisha Saini mkataba huo ,ni mkataba ambao hauna faida yoyote kiuchumi kwa timu”akasema Ochieng’

Timu zote zilizotia saini mkataba huo zimepokea shilingi milioni 2 .

Fkf imeratibu timu za Gor Mahia na Ulinzi Stars kucheza mechi yao ya ufunguzi Jumamosi hii huku Zoo  Fc na Mathare united zikiachwa nje.

Baraza kuu la Fkf linatarajiwa kukutana kuamua hatima ya vilabu hivyo vine huku ikidokezwa kuwa huenda timu hizo zikatimuliwa ligini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *