Zoezi la kukusanya saini milioni 4 kwa ajili ya BBI kuzinduliwa Jumatano

Shughuli ya ukusanyaji saini ili kufanikisha mchakato wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano ya kitaifa, BBI, itazinduliwa Jumatano.

Kulingana na kamati ya kitaifa ya mpango huo wa BBI, shughuli hiyo itatekelezwa kwa muda wa wiki moja, ikilenga kukusanya saini milioni nne.

Kamati hiyo imesema kwamba ripoti ya mwisho ya BBI sasa imekamilika baada ya kuahirishwa wiki iliyopita kufuatia kuchelewa kwa uchapishaji wa mswaada wa marekebisho ya katiba wa mwaka wa 2020.

Wale wanaounga mkono mchakato wa BBI wamehimizwa kujitokeza kwa wingi ili kuweka saini zao katika muda huo wa wiki moja, kamati hiyo ikisema kuwa shughuli ya ukusanyaji saini haiwezi kuahirishwa tena.

Kwengineko Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amepuzilia mbali uwezekano wa ripoti hiyo kufanyiwa marekebisho zaidi, akihoji kuwa tayari meli imeng’oa nanga.

Kwenye mkutano na viongozi wa eneo la Mlima Kenya, Odinga alikiri kwamba ni vigumu kujumuisha marekebisho makuu kwa vile ripoti hiyo imekuwa wazi kujumuisha maoni ya umma kwa zaidi ya miaka miwili.

Viongozi wa eneo hilo wameahidi kuipigia debe ripoti hiyo, wakidai kwamba marekebisho hayo ya kikatiba yatahakikisha usawa katika uongozi wa nchi hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *