Categories
Kimataifa

Zoezi la kuhesabu kura laendelea nchini Uganda

Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea katika baadhi ya vituo vya kupigia kura katika mji mkuu wa Uganda wa Kampala.

Maafisa wa usalama waliongezeka saa ya mwisho kabla ya vituo vya upigaji kura kufungwa saa kumi alasiri.

Malori yaliowabeba wanajeshi yaliendeshwa jijini, ilhali polisi na vitengo vya ulinzi pia walionekana wakishika doria. Katika baadhi ya sehemu, shughuli ya upigaji kura inaendelea.

Kanuni za uchaguzi zinaratibu kuwa watu walioko kwenye milolongo wanaweza kupiga kura baada ya muda rasmi ya kufungwa vituo vya kupigia kura.

Kiongozi wa taifa hilo la Afrika ya Mashariki Yoweri Kaguta Museveni, ameliongoza kwa muda wa miaka 35 sasa huku akijizatiti kuchaguliwa kwa muhula mwingine.

Licha ya kuwa kuna wagombea wengine 10 katika kinyang’anyiro hicho cha urais nchini Uganda, Museveni aliye na miaka 76 anakabiliwa na ukinzani mkali kutoka kwa Bobi Wine mwenye umri wa miaka 38 ambaye ni mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa.

Awali shughuli ya kupiga kura katika ngome ya upinzani ya Masaka nchini Uganda ilichelewa kwa muda licha ya raia kujitokeza kwa wingi mapema asubuhi.

Kuchelewa kwa shughuli hiyo kutokana na agizo la kusitisha huduma za mitandao hapo jana.

Aidha kuna visa kadhaa vya kufeli kwa mitambo ya kutambua wapiga kura kielektroniki.

Mitambo hiyo hutegemea huduma za Internet ambazo zimekatizwa nchini humo huku milolongo ya wapiga kura ikiendelea kurefuka kwenye vituo vya kupigia kura.

Raia wa Uganda waliofanikiwa kupata huduma za Internet walipachika jumbe kwenye mitandao ya kijamii kuelekezea shida zinazowasibu kuwasiliana kwa njia ya rununu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *