Zaidi ya waendeshaji boda boda 4,000 kupewa leseni za kidijitali

Zaidi ya wahudumu 4,000 wa boda boda katika Kaunti ya Laikipia wanatarajiwa kupokea leseni za kidijitali za uendeshaji piki piki.

Mradi huo wa shilingi milioni 40 ulizinduliwa katika Kaunti Ndogo ya Laikipia Mashariki na unalenga kunufaisha wahudumu 7,000 wa boda boda.

Wahudumu hao wataanza kwa kupokea mafunzo kuhusu usalama barabarani kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Akikagua mradi huo, Mbunge wa eneo hilo Amin Mohammed amesema mpango huo ambao ni wa ushirikiano na Halmashauri ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) unalenga kuhakikisha kwamba wahudumu wote wanapata leseni.

Mohammed amesema ukosefu wa leseni kwa wahudumu wa boda boda unatokana na gharama ya juu ya kupata stakabadhi hiyo na umbali wa kusafiri ili kuipata.

Msimamizi wa Halamashuri ya NTSA katika eneo la Kati, Bora Guyo, ametoa wito kwa wahudumu hao kujitokeza kwa wingi.

Wahudumu hao wamesifu huduma hiyo baada ya kusafiri mara kadhaa hadi Kaunti ya Nyeri ili kufikia afisi za Halmashauri ya NTSA.

Wamesema mpango huo utakomesha hali ya kukimbizana na maafisa wa polisi kwa kukosa stakabadhi hitajika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *