Zaidi ya magari 100 ya abiria yanaswa kwa kukiuka masharti ya kudhibiti Covid-19 Kiambu

Msako wa kikosi cha pamoja cha usalama dhidi ya magari ya uchukuzi wa umma yanayokiuka kanuni kuhusu ugonjwa wa COVID-19 umewezesha kunaswa kwa zaidi ya magari 100.

Msako huo uliofanywa katika   kaunti ya Kiambu pasipo wahudumu hao na abiria kutarajia, ulioongozwa na kamishna wa kaunti ya Kiambu Wilson Wanyanga na afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo Ali Nuno, unanuiwa kuhakikisha kanuni za wizara ya afya zinazingatiwa kikamilifu.

Wanyanga alisema msako huo vile vile utatekelezwa katika maeneo ya burudani zikiwemo baa.

Afisa mkuu wa polisi kaunti ya Kiambu Ali Nuno alisema watu wachache hawataruhusiwa kuhatarisha maisha ya mamilioni ya wakenya.

Nuno aliongeza kwamba hawatalegeza juhudi hizo hadi magari ya uchukuzi wa umma yatakapozingatia kanuni za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19.

Baadhi ya madereva waliokamatwa waliikashifu wizara ya afya kwa kujikokota kutoa vyeti vya vipimo vya ugonjwa wa covid-19, huku abiria wakitatizika.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *