Zaidi ya familia 100 zapoteza makao Kwale baada ya nyumba zao kubomolewa

Zaidi ya familia 100 katika eneo la Gombato, Kaunti ya Kwale wameachwa bila makao baada ya makazi yao kubomolewa na mjenzi wa kibinafsi.

Familia hizo zinadai kuwa zimeishi katika ardhi hiyo, ambayo awali ilimilikiwa na waziri wa zamani Darius Mbela, kwa zaidi ya miaka 20 na wamejijengea majumba ya kudumu kwa gharama ya mamilioni ya pesa.

Kulingana na mwenyekiti wa muungano wa maskuota hao, Shaban Luchesi, ubomoaji huo ulitekelezwa katika sehemu ya ardhi ya ekari 1,000 ambayo familia ya Mbela ilimwuuzia mjenzi wa kibinafsi, Harish Patel.

“Tingatinga zilizokuwa zikilindwa na maafisa wa polisi zilikuja katika eneo hili mwendo was aa tisa alfajiri na bila notisi, zikaanza kubomoa nyumba zetu,” amesema Luchesi.

Wakazi hao wameutaja ubomoaji huo kuwa kinyume cha sheria, kwani mahakama iliagiza mnamo mwaka wa 2013 kwamba ekari 100 ya shamba hilo itengewe masquota hao, karibu na Mto Tiwi.

Fatuma Bakari Bundo, ambaye ni muathiriwa, amesema nyumba yao imebomolewa walipokuwa wakilala na watoto wake wanne.

“Baadhi yetu bado tunalipa mikopo ya benki tuliyochukua ili tujenge nyumba hizi,” akalalamika Fatuma.

Seneta wa Kwale Issa Boy amezuru eneo hilo, akashtumu kitendo hicho na kuahidi kuwatafutia haki waathiriwa hao.

Naye Mbunge mpya wa Msambweni Feisal Bader vile vile ameahidi kufuatilia suala hilo na taasisi husika katika kaunti hiyo ili kuhakikisha familia hizo zinafidiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *