Wizara ya Afya yaonya kuhusu ongezeko la vifo vinavyotokana na Corona

Wizara ya Afya humu nchini imeelezea wasi wasi wake kuhusu ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaofariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19 katika siku za hivi karibuni.

Hii ni baada ya wagonjwa 14 kuthibitishwa kuaga dunia kutokana na makali ya ugonjwa huo, masaa 24 yaliyopita, na kufikisha 964, jumla ya wagonjwa waliofariki humu nchini.

Akitoa taarifa ya kuhusu hali ya maambukizi ya ugonjwa humu nchini kutoka Kaunti ya Mombasa, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema nchi hii inashuhudia wimbi la pili la maambukizi hayo lenye athari zaidi ya lile la kwanza.

“Kama mlivyoona, idadi ya maambukizi, wagonjwa walio hospitalini na wale wanaofariki imeongezeka. Tuko katika wimbi la pili la maambukizi ya virusi hivyo humu nchini,” amesema Kagwe.

Amesema kuwa nchi hii imepoteza jumla ya watu 54 ambao wamefariki kutokana na ugonjwa huo ndani ya juma hili pekee.

Waziri huyo pia ametangaza kwamba watu wengine 761 wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19 baada ya sampuli 4,830 kupimwa.

Visa hivyo vipya vimeongeza idadi ya jumla ya maambukizi humu nchini hadi 52,612, baada ya wizara hiyo kupima jumla ya sampuli 678,000 tangu virusi hivyo kuripotiwa.

Kagwe amesema kuwa serikali itatoa muelekeo zaidi kuhusiana na hali ilivyo nchini baada ya kikao kilichoitishwa na Rais Uhuru Kenyatta juma lijalo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *