Will Smith asema yuko tayari kuwania Urais

Muigizaji huyo wa Marekani ambaye pia ni mwanamuziki na mtayarishaji wa filamu alikuwa akizungumza kwenye kipindi cha mitandaoni kiitwacho “Save America” ambacho huendeshwa na Jon Favreau.

Willard Carroll Smith Jr., huchukuliwa na wengi kama mtu ambaye ana ufahamu wa hali ya juu kuhusu uongozi na wanaaminia mawazo yake na huenda isiwe jambo la kushtukizia ikiwa siku moja atawania urais wa Marekani.

Kwenye mahojiano hayo ya jumatatu ambayo lengo lake lilikuwa kutangaza kipindi chake kipya kwenye jukwaa la Netflix kwa jina “Amend: The Fight for America” Will Smith alikiri kwamba hana tatizo lolote katika kuwania uongozi.

Hata hivyo alisema kwa sasa atatoa nafasi kwa afisi hiyo kusafishwa na ataamua baadaye ni wakati gani atatafuta kuingia huko.

Smith alifafanua pia kwamba hata kama atabakia kwenye uigizaji huko Hollywood au ataingilia siasa, atakuwa akitumia jukwaa lake la sasa na ufuasi mkubwa katika kunenea uongozi na kutetea anayoaminia.

Alisema ana maoni kila mara na anaamini na kutumainia kwamba uongozi utakuwa bora kwani anaamini katika maelewano kati ya watu na umoja wa watu.

“Nitatekeleza jukumu langu, iwe ni kupitia sanaa au katika siasa”, Will alisema.

Jarida la PEOPLE lilihusisha muigizaji huyo wa umri wa miaka 52 na wazo la kuingilia siasa na uongozi na kwamba amekuwa akiashiria hayo kwa muda mrefu sasa.

Mwaka 1999 alisikika akitangaza ari ya kuwania urais ambapo alisema kwamba wengi huenda wakapuuza wazo lake lakini anapata nguvu na msukumo kwa viongozi wa awali kama Ronald Reagan.

Muigizaji huyo alisema mwaka 2015 kwamba chuki iliyojitokeza wakati wa kinyang’anyiro cha urais kati ya Donald Trump na Hillary Clinton ilimfanya arejelee wazo la kufuata nyayo za waigizaji wa awali ambao waliingilia siasa na uongozi.

Muigizaji mwingine ambaye ameonyesha nia ya kuwania Urais ni Dwayne “The Rock” Johnson.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *