Categories
Burudani

Wewe ni kakangu, ibaki hivyo! Wendy Williams azomea kakake

Mtangazaji wa runinga nchini Marekani kwa jina Wendy Williams jumatatu asubuhi alianza kipindi chake kwa njia ambayo wengi hawakutarajia.

Aliamua kumjibu kakake Tommy Williams ambaye alikuwa amedai kwamba Wendy hakuhudhuria mazishi ya mama yao mzazi mwezi Disemba mwaka 2020.

Kwenye video hiyo ya You Tube Tommy anasema “Ni nini kitamfanya mtu asihudhurie matanga ya mamake? Sielewi kutompa heshima za mwisho mtu ambaye alikuwa nawe kila wakati na akakusaidia. Unawezaje kuendelea na maisha kana kwamba hakuna kilichotendeka?”

Katika kipindi cha Jumatatu tarehe 18 mwezi Januari mwaka 2021, Wendy Alisema “Nilikuwa napekua mitandao ya kijamii kuona mawazo ya watu kuhusu kipindi chetu cha Wendy Williams Show, kisha nakutana na maneno kama “Ndugu yako hakupendi” mara “Kuwa makini sana na ndugu yako”. Tommy acha nikwambie kitu, wewe ni kakangu, acha kusema unayoyasema kwani sasa yameanza kuingilia kazi zangu.”

Wendy ambaye ni mcheshi alionekana kukasirishwa sana na maneno ya kakake huku akimwonya aache kumwekelea tabia ambayo si yake la sivyo yeye atoe maneno yake ya kweli na ithibati tosha.

“Ukitaka kuzungumza kwenye mitandao sema maneno ambayo unadhani unajua kujihusu.” aliendelea kusema mtangazaji huyo wa miaka 56 sasa na mara moja akageukia kazi ambapo aliuliza watazamaji ikiwa walipenda vazi lake.

Wendy Williams alikuwa na uhusiano mzuri na marehemu mamake kwa jina Mrs Williams ambaye alikuwa akimhusisha kwenye kipindi mara kwa mara.

Wakati mmoja mamake Wendy alihadhithia jinsi kuzaliwa kwa Wendy kuliiletea familia nzima msisimuko maanake walikuwa wanapitia wakati mgumu.

Nyanyake Wendy alikuwa akiugua saratani ya utumbo na aliaga dunia miezi michache baada yake kuzaliwa.

Hata baada ya kuzomewa kwenye runinga, Tommy anaendelea kusisitiza kwamba Wendy hakuhudhuria mazishi ya mama yao. Anasema hata baba yao hakufurahia na jambo hilo linamkwaza hadi sasa.

Anasema alihadaa familia kwamba angesafiri wakati wa mazishi ya mama yao ilhali hakusafiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *