Wenyeji Tanzania kufungua dimba la Cecafa Jumapili
Mashindano ya Cecafa kuwania kufuzu kwa fainali za kombe la Afcon kwa vijana wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka ujao nchini Mauritania yataanza kutimua vumbi Jumapili hii mjini Arusha Tanzania huku mataifa 9 yaliyotengwa katika makundi matatu ya timu tatu kila moja yakiwinda tiketi hizo mbili za Afcon.
Mabingwa watetezi na wenyeji Tanzania almaarufu Ngorongoro Heroes watashuka uwanjani Black Rhino Academy kuanzia saa kumi alasiri siku ya Jumapili Novemba 22 kwa pambano la ufunguzi la kundi A dhidi ya Djibouti.

Sudan kusini itafungua ratiba ya kundi B Jumatatu dhidi ya Uganda wakati Kenya pia ikimenyana na Ethiopia katika mchuano wa Kundi B pia jumatatu.
Mechi za makundi zitakamilika Ijumaa hii Novemba 27 ambapo timu bora kutoka kila kundi na timu ya pili bora kutoka makundi yote matatu zikicheza nusu fainali Novemba 30 ikifuatwa na fainali ya Desemba 2.

Timu mbili bora zitafuzu kwa michuano ya Afcon ya Januari na Februari mwaka ujao nchini Mauritania.
Tanzania waliishidna Kenya bao moja kwa bila katika fainali ya mwaka uliopita nchini Uganda.