Wazito wa Rhumba ambao Watoto walifuata nyayo zao

Muziki wa Rhumba ambao asili yake ni nchini Congo unapendwa sana ulimwenguni kote na vizazi vyote lakini wengi wanaoushabikia ni watu wa umri mkubwa.

Wale ambao walipata nafasi ya kuhudhuria tamasha za wanamuziki kama vile Franco wakiwa vijana. Wengi wa wanamuziki tajika katika fani hiyo wameshaiaga dunia lakini miziki yao bado iko hai.

Huwezi kukosa kumtaja Franco Luanzo Luambo Makiadi unapozungumzia rhumba kwani alitawala muziki nchini Congo kwa muda mrefu na wadadisi wanasema kwamba yeye alikuwa na tabia ya kunyakua kila kipaji kipya ambacho kilikuwa kikichipuza wakati huo na kukiweka chini ya kundi lake la TPOK Jazz.

Hata baada ya kung’aa kwa namna ya kipekee, hakuna mtoto wake, kati ya wote 18, ambaye alifuata nyayo zake katika muziki.

Mwanawe wa kiume kwa Emongo Luambo anaishi mjini Brussels nchini Ubelgiji ambapo anasemekana kuendeleza biashara ya familia yao.

Gwiji mwingine wa muziki wa Rhumba ni Madilu System au ukipenda Jean De Dieu Makiese ambaye alitamba sana. Sio mengi yanafahamika kuhusu familia yake ila inasemekana aliacha mke kwa jina ‘Biya’ na watoto.

Tofauti na hao wawili wa kwanza kulikuwa na Tabuley Rochereau anayefahamika sana kwa kibao “Muzina” ana mtoto ambaye alirithi taaluma yake ya muziki. Mtoto huyo ni wa kiume kwa jina “Pegguy Tabu” ambaye ana kazi nyingi tu za muziki.

Pegguy Tabu

Pegguy pia aliwahi kushirikiana na Koffi Olomide kwa kufanya upya kibao cha marehemu babake kwa jina “Mokolo Nakokufa” maanake “siku nitakufa”.

Pegguy ana kazi nyingine nyingi za muziki. Tabuley aliaga dunia mwaka 2013 lakini mwanamuziki Tshala Muana, ambaye anasemekana kuwa mpenzi wake wakati huo, anahuisha miziki yake ambayo amekuwa akirekodi upya.

Kuna pia daktari wa Rhumba kwa jina Verckys Kiamungana Mateta ambaye sasa ana umri wa miaka 76. Verckys alikuwa mwafrika wa kwanza nchini Congo kumiliki kampuni ya kurekodi muziki na kusimamia wanamuziki. Aliwahi kufanya kazi na Franco kwenye kundi la TPOK Jazz lakini baadaye akaanzisha bendi yake kwa jina ‘Ochestre Veve’ nyingine ‘Ochestre Kiam’ na nyingine ‘Ochestre Lipua Lipua’.

Mwanamuziki huyo mkongwe ana mtoto wa kike kwa jina “Ancy Kiamungana” ambaye pia ni mwanamuziki. Kwa sababu ambazo hazijulikani, mwanadada huyo amezamia tu kufanya marudio ya nyimbo za babake na za wanamuziki wengine maarufu kama Koffi Olomide na Fally Ipupa.

Ancy kiamungana

Ancy na babake Verckys walishirikiana kwa kurudia wimbo wake wa zamani kwa jina “Ngai nakomitunaka”. Sikiliza;

Marehemu M’pongo Love, alipata umaarufu kutokana na kibao chake cha mapenzi kwa jina ‘Ndaya’. Mwanadada huyo aliacha kazi kama karani afisini na kuingilia muziki akiwa bado mdogo ambapo alianzisha bendi kwa jina ‘Tcheke Tcheke Love’ .

Kwenye nyimbo zake, alitetea sana wanawake na kukashifu maswala kama ndoa za wake wengi na tabia ya waume kuweka wake wengine kisiri.

M’pongo Love aliaga dunia mwaka 1990 na aliacha watoto watatu wote wa kike. Kifungua mimba wake Sandra Mpongo anasemekana kujaribu kufuata nyayo za mamake kimuziki na pia ameanzisha wakfu kwa jina la marehemu mamake kwa nia ya kusaidia watoto na wanawake walemavu.

Sandra Mpongo

Christy Lova mtoto wa kike wa Dalienst Ntesa ambaye alikuwa akiimba chini ya kundi la TPOK Jazz naye aliingilia muziki na alijulikana sana baada ya kurudia kibao cha babake kwa jina “Bina na Ngai na Respect” yaani cheza nami kwa heshima.

Kando na kibao hicho, Christy ameimba nyimbo zingine kama vile ‘Mytho’, Dolce vita’, na ‘To Bina’.

Ni baadhi tu ya wanamuziki wa Congo ambao watoto wao wamefuata nyayo zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *