Waziri Mkuu wa Uingereza kutohudhuria ibada ya wafu ya Mwanamfalme Philip

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson hatahudhuria ibada ya wafu ya mumewe Malikia wa Uingereza, Mwanamfalme Philip Jumamosi ijayo.

Hatua hiyo inadhamiria kuruhusu wanafamilia wengi iwezekanavyo kuihudhuria shughuli hiyo kutokana na vizuizi vya kukabiliana na virusi vya korona.

Kulingana na afisi ya Waziri huyo Mkuu, ni watu 30 wakiwemo watoto wa mwendazake, wajukuu na wanafamilia wa karibu ambao wanatarajiwa kuhudhuria shughuli hiyo itakayofanyika kwenye Kanisa la St. George, Windsor.

Raia wameombwa kutoihudhuria hafla hiyo ili kutoa nafasi nyingi kwa wanafamilia wa karibu.

Mrithi wa Ufalme wa Uingereza, Charles ambaye ni mwanawe marehemu alimtaja babake kama mtu mwema  akisema atamkosa babake aliyempenda sana.

Akiongea nyumbani kwake katika eneo la Gloucestershire, Charles alisema marehemu baba yake alikuwa mtu wa kipekee sana.

Philip aliaga dunia katika Jumba la Windsor mnamo Ijumaa, akiwa na umri wa miaka 99.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *