Waziri Macharia afafanua kwa nini chanjo za Korona hazikusafirishwa na Kenya Airways

Waziri wa uchukuzi, James Macharia amesema Shirika la Ndege nchini, Kenya Airways, bado linasubiri ukaguzi wa Shirika la UNICEF ili liruhusiwe kusafirisha chanjo za COVID-19.

Waziri alisema hayo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta alipoandamana na mwenzake wa Afya, Mutahi Kagwe kupokea shehena ya zaidi ya chanjo milioni moja za kukabiliana na maradhi ya COVID-19 za aina ya Oxford-AstraZeneca.

Shehena hiyo iliwasili humu nchini dakika chache kabla usiku wa manane ikiwa kwenye ndege ya Shirika la Ndege nchini Qatar.

Macharia alisema shirika la Kenya Airways tayari limetia saini mkataba na shirika la UNICEF na linasubiri ukaguzi.

Waziri alisema baada ya kuidhinishwa, shirika hilo litajiunga na mashirika mengine ya ndege ulimwenguni kusafirisha chanjo za maradhi ya COVID-19 Barani Afrika.

Shehena hiyo ya zaidi ya chanjo milioni moja ni sehemu ya kwanza ya dozi milioni zilizotengewa nchi hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *