Waziri Amina aungwa mkono Afrika Mashariki kwa cheo cha WTO

Jamii ya Afrika Mashariki imemuunga mkono Waziri wa Michezo humu nchini Balozi Amina Mohammed anayewania nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani, WTO, kufuatia ombi la Rais wa Rwanda Paul Kagame.

Kwenye barua iliyotumwa kwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Adan Mohammed na wenzake wa Rwanda, Burundi, Uganda na Tanzania, Mwenyekiti wa Baraza la Afrika Mashariki Vincent Biruta amesifu mataifa ya jumuiya hiyo kwa kukubali kumuunga mkono mgombea Amina Mohammed.

“Nakujulisha kwamba Balozi Amina Mohammed ameungwa mkono kama mgombea wa Jamii ya Afrika Mashariki katika kuwania nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani,” akasema.

Haya yanajiri huku awamu ya pili ya mashauri kuhusu kumchagua Mkurugenzi Mkuu mpya wa shirika hilo ikifika tamati.

Lengo la mashauri hayo ni kupunguza wagombea waliosalia kutoka watano hadi wawili.

Waziri Amina amekiri kufurahishwa na uungwaji mkono huo.

“Nawashukuru Mawaziri wa Biashara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuunga mkono azma yangu ya kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirika la Biashara Ulimwenguni,” amesema Balozi Amina.

Ameahidi kutumia tajriba yake ya maswala ya biashara na siasa na kuchukua jukumu la kibinafsi kuanzisha mchakato wa mashauri kuhusu mageuzi ya shirika hilo.

“Iwapo nitashinda, nitatumia nguvu zangu zote, ujuzi, elimu na tajriba yangu katika kutekeleza majukumu haya. Kutokana na uzoefu wa kuwa waziri kwa muda mrefu na kuhusika katika mazungumzo ya kimaeneo na kimataifa, nimetayarika kwa majukumu haya,” akaongeza.

Aidha, Amina ameahidi kusaidia mataifa ya Afrika Mashariki kukamilisha mazungumzo kuhusu ruzuku ya sekta ya uvuvi na kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *