Wawili wapatikana na makosa ya kupanga shambulizi la West Gate huku mmoja akiponea

Mahakama imewapata na makosa washukiwa wawili Mohammed Ahmed Abdi na Hussein Mustaffah kwa kuhusika katika shambulizi la kigaidi katika jengo la West Gate mnamo mwaka wa 2013.

Washukiwa hao walishtakiwa kufuatia shambulizi hilo la Al-Shabaab la tarehe 21 Septemba 2013, lililosababisha vifo vya watu 67 na zaidi ya 100 kupata majeraha mabaya.

Hata hivyo, mshukiwa mwengine Abdullah Omar ameachiliwa huru baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kuhusika kwake kwenye shambulizi hilo.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkuu Francis Andayi amesema upande wa mashtaka umetoa ushahidi wa kutosha kuhusu kuhusika kwa Abdi na Mustaffah katika upangaji na kusaidia kundi la kigaidi kutekeleza shughuli zake.

Andayi amesema kuwa licha ya kukana mashtaka dhidi yake, Abdi alipatikana na kipakatalishi kilichokuwa na kanda za video ambazo upande wa mashtaka ulithibithisha kuwa zinaweza kuhusika katika kupanga na kutekeleza vitendo vya ugaidi.

“Nimeona kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka umetosha kukabiliana na kujitetea kwake,” akasema Andayi.

Uamuzi wa mahakama hiyo umeafikiwa kutokana na ushahidi mara 46 wakiwemo mashahidi waliokuwa katika eneo la tukio, maafisa wa usalama na wataalamu wa uchunguzi na ukatosha kuwapata na makosa washukiwa hao wawili katika tukio lililodumu kwa siku nne.

Washukiwa hao walikana mashtaka ya kuhusika kwao lakini mahakama hiyo ikaamua kuwa taarifa zilizopatikana kwenye vifaa vilivyonaswa kutoka kwa gari lililotumika kuwasafirisha wanamgambo wa Al-Shabaab hadi West Gate zinatosha kuwashtaki.

Kulingana na taarifa za uchunguzi, kadi tano za simu zilizopatikana katika gari hilo zilionyesha kuwa waliwasiliana na magaidi hao huku moja kati ya hizo ikiwa na rekodi ya mawasiliano nao mara 226.

Ushahidi huu kulingana na upande wa mashtaka, unabainisha wazi kuwa Abdi na Mustaffah walihusika kikamilifu katika kupanga na kutekeleza shambulizi hilo.

Mshukiwa mwengine wa nne Adan Dhed aliachiliwa mwezi Januari mwaka wa 2019 baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi dhidi yake.

Kundi la Al-Shabaab limelaumiwa kwa kutekeleza mashambulizi katika sehemu mbali mbali nchini Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *