Wavulana 4,000 wakosa kurejea shule huko Baringo baada ya kupashwa tohara

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Dkt. Belio Kipsang amesikitishwa na idadi kubwa ya wanafunzi wavulana katika Kaunti ya Baringo waliokosa kurejea shuleni baada ya kupashwa tohara.

Hii ni baada ya zaidi ya wanafunzi wavulana 4,000 kukosa kuripoti katika shule mbali mbali baada ya kufanyiwa shughuli hiyo ya kitamaduni huku ufunguzi wa shule ukiingia siku ya tatu.

Kwenye ziara yake katika eneo la Baringo Kusini, Katibu huyo amewahimiza wazazi wanaoendelea kutayarisha wavulana wengine kwa tohara wasitishe shughuli hiyo hadi mwezi Aprili.

Ameonya kuwa serikali huenda ikaingilia kati na kulazimika kuwachukulia hatua iwapo wataendeleza zoezi hilo.

Ziara ya Dkt. Kipsang inajiri baada ya taarifa kuwa kundi la wavulana 50 limetayarishwa kwa ajili ya zoezi la upashaji tohara siku ya Jumatano, huku wengine 120 wakitarajiwa kufanyiwa tohara Ijumaa tarehe 16 mwezi huu, wote kutoka kwa jamii ya Ilchamus.

Kipsang pia amesisitiza umakini wa hali ya juu wa serikali kuhakikisha kuhusu kurejea shule kwa wanafunzi wote baada ya kutathmini usalama wa hatua hiyo.

“Tunasubiri muongozo kutoka kwa Wizara ya Afya katika muda wa majuma machache yajayo kabla ya kurejelea masomo kwa wanafunzi wote,” Amesema Katibu Kipsang.

Katibu huyo alikuwa ameandamana na Kamishna wa Kaunti ya Baringo Henry Wafula, Katibu Mkuu wa KUPPET Tawi la Baringo Christopher Kimosop, Naibu Gavana Jacob Chepkwony, miongoni mwa viongozi wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *