Watu wawili wafariki katika ajali ya barabarani Isinya

Watu wawili waliaga dunia katika ajali ya barabarani Jumanne jioni baada ya gari walimokuwa wakisafiria kubingiria mara kadhaa katika eneo la Isinya kwenye barabara ya Nairobi-Namanga.

Ajali hiyo iliyotokea saa kumi na moja jioni, ilihusisha matatu moja ya uchukuzi wa umma na malori mawili.

Kulingana na walioshuhudia ajali hiyo, matatu hiyo iliyokuwa ikielekea Kitengela kutoka Isinya,iligonga lori ambalo lilikuwa limesimama barabarani kabla ya kupoteza mwelekeo na kugonga lori linguine lililokuwa likielekea upande mwingine.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Isinya Kinyua Mugambi,alidhibitisha ajali hiyo huku akitoa wito kwa madereva kuwa waangalifu sana barabarani.

Mugambi alisema kuwa ajali hiyo ingeepukika iwapo dereva huyo angekuwa makini.

“Lori hilo ambalo lilikuwa limesimama barabarani liliweka alama za kuokoa maisha na pia matawi yalipangwa barabarani kuwatahadharisha madereva, lakini dereva wa matatu hiyo alipita na kugonga lori hilo,”alisema Mugambi.

Aliwaonya madereva dhidi ya kuendesha magari kwa kasi kupita kiasi huku akiwahimiza abiria kufunga mikanda ya usalama kwani huwasaidia kuokoa maisha yao.

Maiti ya wawili hao ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kajiado.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *