Watu 80 zaidi waambukizwa Corona Kenya

Wizara ya Afya imethibitisha visa vipya 80 vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 kutokana na upimaji wa sampuli 1,601 katika muda wa masaa 24 yaliyopita.

Visa hivyo vimefikisha jumla ya maambukizi humu nchini hadi 95,923 baada ya jumla ya sampuli 1,033,322 kufanyiwa uchunguzi tangu kisa cha kwanza kuthibitishwa humu nchini mwezi Machi.

Kati ya visa hivyo, 63 ni vya Wakenya ilhali 17 ni raia wa kigeni, 51 kati yao wakiwa ni wanaume nao 29 ni wanawake, wote wa kati ya umri wa miaka mitatu hadi 98.

Kaunti ya Nairobi ndiyo iliyoripoti visa vingi zaidi (55), ikifuatwa na Busia kwa visa 7, Lamu 5, Kiambu 4, Murang’a 3, Kilifi 2, huku Kajiado, Kericho, Kitui, na Nakuru zikiripoti kisa kimoja kimoja.

Wizara hiyo pia imethibitisha kupona kwa wagonjwa 425. Kati ya hao, 369 walikuwa kwenye mpango wa kuhudumiwa nyumbani ilhali 56 walikuwa wakitibiwa hospitalini.

Hii imefanya idadi ya waliopona kuwa 77,423.

Hata hivyo, wagonjwa watatu wamefariki kutokana na makali ya COVID-19 na kuifanya jumla ya waliofariki humu nchini kuwa 1,658.

Hadi sasa, jumla ya wagonjwa 651 wanatibiwa katika vituo mbali mbali vya afya humu nchini nao 3,417 wanahudumiwa nyumbani.

Wagonjwa 38 wako kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi, 18 kati yao wakiwa wanasaidiwa kupumua huku 17 wakiwa wanapokea hewa ya ziada ya Oksijeni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *