Watu 337 wahukumiwa vifungo vya maisha gerezani nchini Uturuki

Mahakama moja nchini uturuki imewahukumu vifungo vya maisha gerezani maafisa 337 wa kijeshi pamoja na watu wengine katika mojawapo wa kesi kubwa zaidi zinazohusiana na jaribio la mapinduzi ya serikali mwaka 2016.

Marubani wa ndege za vikosi vya angani na makamanda wa kijeshi ni miongoni mwa takriban washtakiwa 500 walioshtakiwa kwa kujaribu kupindua serikali ya rais  Recep Tayyip Erdogan.

Yadaiwa kwamba waliongoza njama hiyo kutoka kwenye kituo cha jeshi la angani cha  Akinci viungani mwa jiji kuu Ankara.

Erdogan alisema kuwa mhubiri mmoja wa kiislamu aliye nchini marekani kwa jina Fethullah Gulen alipanga njama hiyo iliyowafanya watu wengi kukamatwa.

Gulen amekanusha kuhusika kwenye jaribio hilo la kupindua serikali lililotekelezwa mwezi Julai mwaka 2016 lililosababisha vifo vya watu 251 huku wengine zaidi ya elfu-2 wakijeruhiwa.

Kesi hiyo ilianza mwezi Agosti mwaka 2017 ambapo mashtaka ni pamoja na kutaka kumuua rais Erdogan na kuteka taasisi kuu za kiserikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *