Watu 329 zaidi wapona Covid-19 huku 176 wakiambukizwa virusi hivyo nchini

Wagonjwa 329 wamepona ugonjwa wa COVID-19 humu nchini katika muda wa saa 24 zilizopita, na kuongeza jumla ya idadi ya wagonjwa waliopona ugonjwa huo humu nchini kufikia 22,771.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumamosi alaasiri iliyotiwa saini na waziri wa afya Mutahi Kagwe ,Wizara ya afya imesema 43 kati ya wagonjwa hao ni wale waliokuwa wakihudumiwa chini ya mpango wa utunzi wa nyumbani na 286 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbali mbali humu nchini.

Kagwe amesema wagonjwa watatu Zaidi wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo na kuongeza idadi ya watu ambao wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo humu nchini kufikia 619.

Katika muda wa saa 24 zilizopita, watu 176 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya korona  na kuongeza idadi ya watu waliodhibitishwa kuambukizwa virusi hivyo humu nchini kufikia jumla ya watu 35,969.

Kulingana na Kagwe,visa hivyo vipya vimethibitishwa baada ya sampuli 4,115 kupimwa katika muda wa saa 24 zilizopita.

Kati ya visa hivyo vipya 171 ni wakenya ilhali watano ni raia wa kigeni.132 ni wanaume na 44 wanawake.

Wizara ya afya imesema kaunti ya Nairobi inaendelea kuongoza kwa visa 32 ikifuatiwa na kaunti ya Nakuru kwa visa 29, Mombasa 22 Kajiado 14 Kisii 9, Kiambu 7.

Garissa,  Nyeri, Migori, Kisumu na Vihiga zilinakili visa sita kila moja.

Jumla ya sampuli 494,560 zimepimwa tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa wa COVID 19 kuripotiwa humu nchini mwezi March mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *