Watu 3,000 walifariki kutokana na saratani ya mlango wa uzazi mwaka 2020 nchini

Kenya ni miongoni mwa mataifa 20 yanayoathirika zaidi kutokana na saratani ya mlango wa uzazi kote duniani.

Takriban visa vipya  5,236 vilinakiliwa mwaka 2020 ambapo watu 3,211 walifariki kutokana na ugonjwa huo.

Hata hivyo idadi ya wanawake na wasichana ambao wamefanyiwa uchunguzi wa ugonjwa huo ni chini ya asilimia 16.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa wiki ya uhamasishaji wa kitaifa kuhusu saratani ya mlango wa uzazi mjini  Nanyuki, mkurugenzi wa huduma za kuzuia magonjwa katika idara ya huduma za matibabu Dkt. Pacifica Onyancha alisema saratani ya mlango wa uzazi ni moja ya aina za saratani zinazoweza kuzuiwa zaidi na hakuna mtu anayestahili kufariki kutokana nayo.

Dkt. Onyancha ambaye alimwakilisha waziri wa afya Mutahi Kagwe alisema saratani ya mlango wa uzazi ina tiba na inaweza kuzuiwa kwa kutumia chanjo ya HPV, inapatikana bila malipo hapa nchini kwa wasichana wa umri wa miaka kumi.

Aidha uchunguzi wa mara kwa mara wa saratani ya mlango wa uzazi kwa wanawake unaweza kusaidia kuzuia kufikia viwango visivyoweza kutibika.

Daktari huyo alisema ipo haja ya kuchukua hatua ya kuzuia maambukizi na vifo vinavyotokana na saratani hiyo kwa hadi asilimia 50  kufikia mwaka 2030.

Kwa ujibu wa Dkt Onyanch,chanjo ya  HPV inayotolewa kwa wasichana wa umri mdogo hapa nchini si aina ya mbinu ya upangaji uzazi, bali ni hatua ya serikali na wadau wengine katika sekta ya afya ya kuzuia ugonjwa huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *