Watu 271 zaidi waambukizwa Covid-19 nchini

Visa vya virusi vya Covid-19 ambavyo vilionekana kupungua humu nchini katika siku za hivi karibuni, sasa vinaonekana kuongezeka tena.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema virusi vya corona vinaenea kwa haraka kote nchini huku visa 271 vipya vikithibitishwa Alhamisi.

Visa hivyo vipya vimetokana na kupimwa kwa sampuli 5,034 katika muda wa saa 24 zilizopita na kufikisha idadi jumla ya visa vya Covid-19 humu nchini 40,178.

“Katika muda wa wiki mbili zilizopita tumeshuhudia mfumo mpya wa msambao wa Covid-19 humu nchini. Kaunti kadhaa ambazo ziliandikisha idadi ndogo kama vile Trans Nzoia, ghafla zimeanza kunakili idadi ya huu ya maambukizi,” alisema waziri huyo wa Afya.

Kulingana na Kagwe kwa sasa kaunti ya Trans Nzoia imeorodheshwa ya 18 kati ya kaunti zote 47 ikiwa na visa.

Alisema idadi hiyo mpya inapaswa kuwa onyo kwa wakenya akisema iwapo hali hiyo haitadhibitiwa huenda taasisi za afya zikafurika.

Kagwe alisema mikutano ya kisiasa na mikusanyiko ya umma itachangia zaidi kuenea kwa virusi hivyo hatari.

Kati ya visa hivyo vipya vilivyotangazwa Alhamisi, 242 ni wakenya ilhali 29 ni raia wa kigeni.

177 ni wa kiume huku 94 wakiwa wa kike. Mwathiriwa mchanga zaidi ana umri wa mwaka mmoja huku mkongwe zaidi akiwa na miaka 83.

Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa visa 81, Mombasa 58, Turkana 16, Kisumu 15, Garissa 13, Kiambu 13, Kisii 10, Machakos 10, Laikipia 8, Nandi 6, Nakuru 6, Uasin Gishu 5, Kilifi 5, na Muranga 5.

Kaunti ya Nyamira  na  Siaya  zilinakili visa 4 kila moja

Kaunti ya Kakamega, Kajiado, Kwale, Migori, Homabay, Embu , Narok na Meru zilinakili kisa kimoja kila moja.

Watu watatu zaidi wameaga dunia kutokana na covid-19 humu nchini na kufikisha idadi jumla ya maafa humu nchini kutokana na virusi hivyo kuwa 751.

Hata hivyo watu wengine 51 wamepona virusi hivyo, 29 kutoka taasisi mbali mbali za afya huku 22 wakitoka katika mpango wa utunzi wa wagonjwa nyumbani.

Idadi jumla ya waliopona Covid-19 humu nchini sasa ni watu  31,710.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *