Watu 14 zaidi wafariki huku wengine 968 wakiambukizwa virusi

Kenya imenakili visa vipya 968 vya maambukizi ya virusi vya korona kutokana na sampuli 6,610 zilizopimwa.

Jumla ya visa 77,372 vya maambukizi ya korona vimethibitishwa hapa nchini tangu kubainishwa kwa kisa cha kwanza mwezi Machi mwaka huu.

Kati ya visa hivyo vipya, 888 ni Wakenya ilhali 80 ni raia wa kigeni.

Kijinsia, 584 ni wanaume na 384 ni wanawake, huku mgonjwa wa umri mdogo akiwa mtoto wa miezi miwili na yule wa umri mkubwa akiwa na miaka 91.

Kaunti ya Nairobi kwa mara nyingine imeongoza kwa maambukizi mapya kwa kunakili visa 421, ikifawtiwa na Mombasa kwa visa 91, Kilifi 88, Busia 73, Kiambu 54 na Kajiado visa 30.

Wagonjwa 1,131 wamelazwa katika vituo mbali mbali vya afya, 63 katika vyumba vya matibabu maalumu, 36 wanatumia vipumuzi na 26 wanaongezewa hewa ya oksigeni.

Hayo yamejiri huku wagonjwa 155 wakipona, 110 chini ya mpango wa uuguzi wa nyumbani na 45 katika vituo mbali mbali vya afya nchini.

Watu wengine 14 wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo na kuongeza idadi jumla ya vifo hadi 1,380.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *