Watu 129 zaidi waambukizwa Covid-19 hapa nchini

Kiwango cha maambukizi ya virusi vya Covid-19 hapa nchini kimeshuka hadi asilimia 2.5 baada ya watu wengine 129 kuambukizwa virusi hivyo.

Idadi hiyo ya Jumamosi ilinakiliwa baada ya kupimwa kwa sampuli 5,091 katika muda wa saa 24 zilizopita.

Idadi jumla ya maambukizi ya virusi vya Covid-19 hapa nchini sasa ni 99,898.

Kati ya visa hivyo vipya 108 ni wakenya ilhali 21 wakiwa raia wa kigeni huku 79 wakiwa wa kiume na 50 wa kike.

Mwathiriwa mchanga zaidi ni mtoto wa umri wa miezi mitatu na yule mkongwe zaidi ana umri wa miaka 83.

Kulingana na taarifa ya wizara ya afya, wagonjwa 70 wamepona virusi hivyo hatari ambapo 44 wameruhusiwa kuondoka kutoka vituo mbali mbali vya afya na 26 kutoka mpango wa kuwatunza wagonjwa wa corona nyumbani.

Kaunti ya Nairobi iliongoza katika maambukizi ya visa vipya  huku ikinakili visa 81. Kaunti za Kiambu na Mombasa zilifuata kwa visa 8 kila moja.

Nakuru iliandikisha visa 5 huku Kilifi na Kajiado zikiwa na visa 4 kila moja.

Uasin Gishu na Kitui zilinakili visa 3 kila moja, Turkana 2 nazo Homabay, Kisii, Machakos na Meru zikiandikisha kisa kimoja kila moja.

Jumla ya wagonjwa  541 wa COVID-19 wamelazwa katika vituo mbli mbali za afya kote nchini huku 1,564 wakitunzwa nyumbani.

Wagonjwa 27 wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ambapo 16 wanatumia vipumulio na wengi 10 wanapokea hewa ya oxygen ya ziada.

Jambo la kutia moyo ni kwamba hakuna kifo kimeripotiwa kutokana na Covid-19 hapa nchini katika muda wa saa 24 zilizopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *