Watu 123 wathibitishwa kuambukizwa COVID-19, huku wagonjwa 412 wakipona

Wizara ya Afya humu nchini imenakili visa vipya 123 vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 na kufikisha idadi jumla ya maambukizi ya ugonjwa huo kuwa 98,555.

Kulingana na taarifa ya Alhamisi kuhusu hali ya janga la Corona, visa hivyo vipya vimetokana na sampuli 4,948 zilizopimwa katika muda wa masaa 24 yaliyopita. Hii imefikisha jumla ya sampuli zilizopimwa humu nchini hadi 1,102,595.

Visa hivyo vipya vinajumuisha Wakenya 111 na raia 12 wa kigeni, wanaume 74 na wanawake 49, wa kati ya umri wa mwaka mmoja hadi miaka 85.

Kulingana na Waziri wa Afya Mutahi kagwe, wagonjwa 412 wamepona, 378 kati yao walikuwa kwenye mpango wa kutibiwa nyumbani ilhali 34 walikuwa hospitalini.

Jumla ya waliopona kutokana na COVID-19 kufikia sasa ni 81,667.

Kagwe pia amethibitisha kufariki kwa wagonjwa wanne na kufikisha idadi ya waliofariki hadi 1,720.

Kufikia sasa, jumla ya wagonjwa 675 wanatibiwa katika vituo mbali mbali vya afya humu nchini, huku 1,945 wakihudumiwa nyumbani.

Wagonjwa 26 wako katika vyumba vya wagonjwa mahututi, 17 kati yao wanasaidiwa kupumua huku 8 wakiwa wanapokea hewa ya ziada ya Oksijeni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *