Watu 1,130 zaidi waambukizwa Covid-19 hapa nchini

Serikali imeeleza wasiwasi kuhusiana na ripoti kuwa baadhi ya taasisi za kiafya zinawafukuza wahudumu wa afya wanaotaka kuchanjwa dhidi ya virusi vya corona na ambao wanafanya kazi katika hospitali nyingine tofauti.

Akiongea katika jumba la Afya wakati wa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya virusi vya corona nchini, waziri wa afya Mutahi Kagwe aliagiza maeneo yote ya kutoa chanjo kutoa kipau mbele wafanyikazi wa mstari wa mbele bila mapendeleo yote.

Kagwe, hata hivyo alitoa wito kwa vituo vyote vya afya kunakili kila chanjo ili kuhakikisha kuwepo kwa uwazi.

Alionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya hospitali ambazo hazitatoa hesabu sahihi ya chanjo zilizotolewa.

Haya yanawadia huku kiwango cha maambukizi kikiendelea kuongezeka baada ya watu 1,130 kupatikana kuwa na virusi vya corona katika muda wa saa 24 zilizopita baada ya kupimwa kwa sampuli 5,119.

Hii inafikisha idadi jumla ya maambukizi kuwa watu 122,040.

Watu 12 walifariki kutokana na virusi hivyo na kufikisha idadi jumla ya waliofariki kuwa watu 2,023.

Nairobi iliongoza katika maambukizi ya visa vipya vya Covid-19, huku ikinakili visa 730, ikifuatwa na  Kiambu kwa visa 118, Machakos ilikuwa na visa 60, Kajiado 33, Nakuru 30, Meru 24, Uasin Gishu 23, Laikipia 19, Mombasa 14 na Murang’a visa 10.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *