Watoto wawili wauawa na Kiboko ufuoni Ziwa Victoria

Watoto wawili wamefariki baada ya kushambuliwa na Kiboko katika maeneo ya Siungu na Uhwaya kwenye fuo za Ziwa Victoria, Kaunti Ndogo ya Bondo.

Katibu wa kikundi cha usimamizi wa eneo la ufuo la Siungu, Erick Ochieng, amesema watoto hao walikuwa wakioga katika eneo hilo la ufuo wakati waliposhambuliwa na Kiboko.

Ochieng amesema mnyama huyo alimshambulia mtoto wa kwanza mvulana, ambaye alikuwa wa gredi ya kwanza, katika ufuo wa Siungu kabla ya kuelekea eneo jingine la ufuo wa Uhwaya ambako pia alimshambulia na kumjeruhi vibaya mvulana mmoja wa darasa la nane, ambaye anaendelea kutibiwa katika hospitali moja ya sehemu hiyo.

Amesema mtoto wa tatu ambaye aliumwa tumboni na mnyama huyo huyo, alitangazwa kuwa amefariki baada ya kufikishwa kwenye kituo cha afya cha Got Agulu.

Wavuvi katika eneo hilo wametoa wito kwa serikali kuingilia kati kupitia kwa Shirika la Huduma kwa Wanyama Pori nchini (KWS), ili kuhakikisha mnyama huyo amenaswa ama kuhamishwa katika juhudi za kukomesha mizozo kati ya wanadamu na wanyama katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *