Watetezi wa haki watakiwa kumuokoa msichana anayeteswa na babake wa kambo Bunyala

Watetezi wa haki za binadamu na wahisani wametakiwa kuingilia kati na kumuokoa msichana mmoja mwenye umri wa miaka 19 kutoka kijiji cha Mahoma katika eneo la Bunyala kufuatia madai ya kudhulumiwa na baba yake wa kambo.

Mitchel Nerima, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Mahoma, amesemekana kunyanyaswa na kudhulumiwa pakubwa, hali iliyomfanya kutoroka nyumbani.

Kwa mujibu wa msichana huyo, baba wake wa kambo ambaye ni mlevi huzozana na mama yake kila anaporejea nyumbani huku hasira zake zikiishia katika kumcharaza Nerima.

Nerima anasemekana kutorokea Tanzania miezi minne iliyopita ili kutafuta kazi za nyumbani na baadaye akaokolewa na wahisani ambao walimrejesha nyumbani.

Victor Ngosia, ambaye ni Naibu Mwalimu Mkuu alielezea kusikitishwa na masaibu ambayo msichana huyo amekuwa akipitia, huku akitoa wito kwa wazazi wake kurekebisha hali hiyo na kumpa msichana huyo mazingira bora ya kukua.

“Naomba wazazi tuwape nafasi wanafunzi wote wasome ili ndoto zao zitimie. Iwapo kuna changamoto yoyote ile, nawarai wazazi wawe wazi ili wahusika waingilie,” akasema Ngosia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *