Watafiti wa humu nchini wapewa changamoto ya kutafuta suluhu ya janga la COVID-19

Katibu wa Elimu ya Vyuo Vikuu na Utafiti Balozi Simon Nabukwesi amewambia Wanasayansi na watafiti kuwianisha tafiti zao na mbinu za kutafuta suluhisho kwa changamoto za kijamii kama vile ugonjwa wa COVID-19.

Amewataka watafiti kutumia muda wao kupambanua changamoto zinazokumba jamii na kutumia uwezo wao wa kifikra kukabiliana na changamoto za kila siku.

Nabukwesi amewataka wanasayansi kubuni njia za kupambana na ugonjwa wa COVID-19 kwa kushirikisha maarifa yao na ya wengine.

Ametaja mfano wa Afrika Kusini ambayo inakusanya takwimu kila siku wakati wa uchunguzi kuhusu ugonjwa wa Covid-19 na kufanya tathmini kuhusu jinsi ya kuimarisha mbinu za kukabiliana na janga hilo.

Balozi Nabukwesi amesisitiza haja ya kubadili itikadi za kitamaduni na kihisia ili kuibuka kuwa watafiti bora.

Nabukwesi aliyasema hayo huko Mombasa wakati wa kufunga warsha ya siku tatu yenye kauli mbiu ya “Sayansi na teknolojia, muitikio wa ubunifu kwa janga la COVID-19 na mbinu za kulikabili”.

Warsha hiyo iliandaliwa na Tume ya kitaifa kuhusu sayansi, teknolojia na ubunifu, NACOSTI.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *