Wasafi Tv yafungwa kwa miezi sita

Kituo cha runinga kwa jina Wasafi Tv cha Tanzania kinachomilikiwa na mwanamuziki Diamond Platnumz kimefungiwa kisipeperushe vipindi na matangazo kwa muda wa miezi sita na mamlaka ya mawasiliano nchini humo TCRA.

Inasemekana kwamba kituo hicho kilikiuka kanuni na maadili wakati kilipeperusha tamasha moja mubashara ambapo msanii kwa jina Gigy Money alionyeshwa akiwa uchi jukwaani wakati wa tamasha la Wasafi Media huko Dodoma.

Msanii Gigy Money naye amezuiwa kujihusisha na shughuli zote za sanaa kwa muda wa miezi sita.

Kaimu mkurugenzi wa TCRA Bwana Johannes Kalungule ndiye alitangaza hayo na kuutaka usimamizi wa kituo hicho cha runinga kuomba umma msamaha.

Kulingana na Kalungule uamuzi huo wa kukifunga kituo hicho cha runinga uliafikiwa baada ya mkutano kati ya pande hizo mbili.

Kufikia sasa usimamizi wa kituo hicho haujasema lolote hata kuomba msamaha kulingana na maagizo.

Hii sio mara ya kwanza kampuni ya Wasafi inajipata pabaya, mwaka jana kituo chake cha redio kwa jina Wasafi fm kilifungiwa kwa muda wa siku saba kwa sababu sawia ya kukiuka maadili.

Marufuku hiyo ilianza kutekelezwa tarehe 12 mwezi septemba mwaka jana na usimamizi wa kituo hicho uliamua kupeleka watangazaji wake katika eneo la wasafi village ambapo walikumbushwa maadili ya kazi na kupata muda pia wa kujiliwaza.

Watangazaji wa vipindi vya “The Switch” na “Mashamsham” wanasemekana kutumia maneno ambayo yalikuwa kinyume na maadili kati ya tarehe mosi na tarehe nne mwesi Agosti mwaka 2020.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *