Wapenzi wa BBI kuanza kukusanya saini milioni moja wiki hii

Wakenya wanaounga mkono ripoti ya mpango wa maridhiano ya kitaifa, BBI, wanatarajiwa wiki hii kuanza kukusanya saini milioni moja.

Kwa mujibu wa ripoti rasmi, shughuli ya ukusanyaji saini hizo zitakazowezesha katiba kufanyiwa marekebisho itazinduliwa kesho.

Siku ya Ijumaa, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga aliwaambia wanahabari kuwa  anatarajia shughuli hiyo kutekelezwa katika muda wa siku 30 ili kutoa fursa ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi mwezi Juni mwaka ujao.

Ukusanyaji wa saini hizo utakapokamilika, zitawasilishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, pamoja na nakala ya ripoti ya BBI kwa uthibitisho.

Baadaye itapelekwa kwa mabunge yote 47 ya kaunti ili ijadiliwe na kupitishwa.

Ikiwa bunge la kaunti litaidhinisha mswada huo, spika atawasilisha nakala yake kwa maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti na cheti cha kuonyesha umepitishwa.

Ikiwa mswada huo utapitishwa na mabunge mengi ya kaunti, utawasilishwa mara moja kwenye Bunge la Kitaifa.

Mswada huo ukipitishwa na wabunge wengi katika mabunge mawili ya kitaifa, utapelekewa rais kuidhinishwa kuwa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *