Wanyakuzi wa ardhi Kajiado kuchukuliwa hatua kali

Gavana wa Kaunti ya Kajiado Joseph Ole Lenku amesema kuwa serikali yake itamchukulia hatua za kisheria yeyote atakayepatikana akijihusisha na unyakuzi wa ardhi katika kaunti hiyo.

Lenku amewaonya vikali wanaojipatia hati miliki za ardhi kwa njia ya ulaghai na kupuuzia sheria za kaunti hiyo kuhusu uuzaji na ununuzi wa ardhi.

Licha ya serikali hiyo kuunda sheria kali zilizolenga kukabiliana na mizozo ya ardhi miaka miwili iliyopita, watu wameendelea kulaghaiwa kwenye mchakato wa ununuzi wa ardhi katika sehemu hiyo.

Kulingana na Gavana Lenku, mizozo ya ardhi imezidi kukithiri miongoni mwa jamii za Kajiado, huku kesi nyingi zikiwa za wale wanaojaribu kumiliki tena ardhi za kifamilia ambazo ziliuzwa na wazazi wao kiholela.

Hata hivyo, aliyekuwa Mwakilishi Wadi ya Kitengela na Wakili wa Mahakama Kuu Daniel Kanchori amewalaumu wakuu katika afisi za ardhi za kaunti hiyo wanaoendeleza ufisadi kwenye maswala ya ardhi, akisema kuwa wamechangia katika visa vingi vya mizozo ya ardhi.

Kanchori amesema maafisa hao wamekuwa wakipokea hongo ili kufanya usajili wa ardhi kinyume cha sheria na kusababisha wakazi wengi kupoteza vipande vyao vya ardhi.

“Maafisa wengi wanaoletwa Kajiado, badala ya kuhudumia wananch, wanaingia katika biashara hiyo ya mashamba,” amesema Kanchori.

Amesema iwapo sheria za ardhi za kaunti hiyo zitatekelezwa kikamilifu, visa vya ulaghai na mizozo ya ardhi vitapungua kwa kiasi kikubwa katika kaunti hiyo.

Hivi majuzi, maafisa wa ardhi walikamatwa katika Afisi ya Ardhi iliyoko Ngong wakiwa na hati miliki bandia katika msako uliotekelezwa kufuatia malalamishi ya muda mrefu kutoka kwa umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *