Wanjiru atwaa ubingwa wa mbio za nyika za Magereza

Rosemary Wanjiru ndiye bingwa wa mwaka huu katika mbio za nyika za kilomita 10 za  idara ya  magereza   zilizoandaliwa mapema Jumamosi katika uwanja wa chuo cha mafunzo ya makurutu wa magereza KPTC mjini Ruiru.

Wanjiru ambaye aliibuka wa nne katika  mbio za mita 10000 kwenye  mashindano ya dunia ya mwaka 2019 mjini Doha  Qatar, alistahimili ushindani mkali  kutoka kwa mshindi wa nishani ya shaba  ya dunia ya mbio za nyika  mwaka 2017 Lillian Kasait Lengurok na kukata utepe kwa dakika 33 sekunde 43 nukta 53 .

Kasait aliibuka wa pili kwa dakika 34 sekunde 17 nukta  01 , akifuatwa na Gladys Cherono kwa dakika 25 sekunde 7 nukta 24 ,naye bingwa wa dunia wa mbio za Nyika mwaka 2017  Alice Aprot aliyekuwa akirejea  kwa mara ya kwanza baada ya likizo ya kujifungua akiridhia nafasi ya 4  kwa dakika 35 sekunde 55  nukta 24, wakati bingwa mtetezi Leicester Chemening akifunga ukurasa wa tano bora kwa dakika  35 sekunde 58 nukta 52 .

Wanariadha bora watakaochaguliwa wataiwakilisha idara ya magereza kwenye mashindano ya kitaifa ya mbio za nyika mwezi ujao  huko Kisii Golf Club ambapo chama cha riadha Kenya kitateua timu itakayoshiriki mashindano ya Afrika ya mbio za Nyika mjini Lome Togo mwezi Machi mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *