Wanawake Tana River wajitosa kutetea nafasi za uongozi serikalini

Wanawake wataalamu katika Kaunti ya Tana River wameanzisha mchakato wa kushinikiza kujumuishwa kwenye nyadhifa za uchaguzi na uteuzi serikalini.

Kupitia mpango wa ‘Tana River County Women for Change’, kundi hilo linanuia kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi sawa na wenzao wanaume kuwakilisha kaunti katika viwango viwili vya serikali.

Wanawake hao ambao walihudhuria mafunzo ya siku mmoja kuhusu uongozi yalioandaliwa na chama cha wanawake mawakili FIDA katika Hoteli ya Ocean Beach mjini Malindi, wanasema wamebakia nyuma kutokana na imani za kitamaduni ambazo zinawatambua wanaume pekee.

Mwenyekiti wa mpango huo Hadia Komora amesema wanataka kuwapa wanawake uwezo katika kaunti ili waweze kutetea haki zao.

Komora ameahidi kumuunga mkono mwanamke yeyote ambaye atawania wadhifa wa uchaguzi kwenye uchaguzi mkuu mwaka wa 2022.

“Mama yeyote tutakayemuona anapigania wadhifa wa uchaguzi au uteuzi, tutamsaidia na kusimama naye,” ameahidi Komora.

Naye Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Tana River Rehema Hassan amesema pendekezo la marekebisho ya katiba kupitia BBI huenda likaathiri uongozi wa akina mama hasa ikiwa nafasi ya mwakilishi wa wanawake Bungeni itaondolewa.

“Kama si hii katiba, hakuna mwanamke wa Tana River angeonekana Bungeni. Vile tunaona nafasi ya mwakilishi wa wanawake huenda kikatolewa, tunaona tutakosa uwakilishi,” akasema Bi. Hassan.

Bi. Hassan amesema kwa sababu Bunge limeshindwa kupitisha sheria ya thuluthi mbili ya usawa wa jinsia, wanawake sasa wamejiunga ili kutetea uongozi kupitia uchaguzi katika nafasi mbali mbali serikalini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *