Wananchi wa Guinea wapiga kura kumchagua rais

Raia wa Guinea wanapiga kura kwenye uchaguzi wa urais leo huku Rais Alpha Condé mwenye umri wa miaka 82 akitaka awamu ya tatu.

Muda wa kampeni ulikamilika Ijumaa usiku wa manane katika nchi hiyo huku kukiwa na wasi wasi wa kuzuka kwa vita baada ya kundi la watu wasiojulikana kuvamia kambi ya kijeshi nchini humo na kumwua kwa kumpiga risasi afisa mkuu wa kijeshi.

Rais Condé alishinikiza kupitishwa kwa katiba mpya mwezi Machi akisema katiba hiyo itaboresha nchi hiyo, hatua ambayo pia ilimwezesha kukwepa sharti la rais kuhudumu kwa hatamu mbili.

Baada ya kuwa mwanaharakati wa upinzani kwa miongo kadhaa , Condé aliibuka kuwa rais wa kwanza  Guinea kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia mwaka 2010 na akashinda uchaguzi mwingine ulioandaliwa mwaka  2015.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakimkosoa rais huyo huku wakimtuhumu kwa kuwa dikteta.

Condé anakabiliana na mpinzani wake wa muda mrefu Cellou Dalein Diallo, ambaye tayari amemshinda katika chaguzi mbili.

Diallo, mwenye umri wa miaka 68, ambaye sasa ndiye kiongozi wa upinzani nchini  Guinea alikuwa waziri mkuu chini ya aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Lansana Conté.

Takriban wapiga kura mlioni 5.4 wanashiriki katika zoezi hilo huku matokeo yakitarajiwa kutangazwa baada ya siku chache.

Ili kushinda urais moja kwa moja, mgombea anatakiwa kupata zaidi ya nusu ya kura hizo, vyenginevyo kutakuwa na awamu ya pili ya kura ya urais mnamo tarehe 24 Nonvemba mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *