Wanakandarasi wanaotengeneza madawati ya shule watakiwa kuzikamilisha kwa wakati

Wanakandarasi wanaotengeneza madawati ya shule chini ya mpango wa ufufuzi wa kiuchumi wameagizwa waharakishe shughuli hiyo la sivyo wapokonywe kandarasi hizo.

Kamishna wa kaunti ya Kilifi Kutswa Olaka alisema kuwa madawati 9,450 na mashubaka 6,850 kwa shule za msingi na sekondari mtawalia ni sharti yawe tayari kwa matumizi kufikia mwishoni mwa juma lijalo.

Akiongea mjini Malindi alipokuwa kwenye ziara ya ukaguzi wa karakana zinazotengeneza madawati hayo chini ya mpango huo, kamishna huyo aliagiza kamati za kaunti ndogo kusimamia shughuli hiyo na kuhakikisha agizo hilo linatimizwa.

Olaka alilalamika kwamba wanakandarasi wengi waliopewa zabuni za kutengeneza madawati hayo katika kaunti ndogo ya Malindi huenda wasikamilishe kazi hiyo katika muda uliokubaliwa huku wengine wakitakiwa kurekebisha kazi yao kabla ya kuziwasilisha.

Serikali inatarajiwa kutumia shilingi milioni 61.56 kutengeneza madawati 70 kwa kila mojawapo wa shule 135 za msingi zilizoteuliwa na mashubaka 50 kwa kila mojawapo wa shule za sekondari katika kaunti ya Kilifi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *