Wanakandarasi Kisumu walalamikia kucheleweshwa kwa malipo yao

Wanakandarasi katika Kaunti ya Kisumu wameitaka serikali ya kaunti hiyo kuwalipa malimbikizi ya madeni ya mamilioni ya pesa.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wao Maurice Aloo, wanakandarasi hao wameshtumu usimamizi wa kaunti hiyo kwa kupuuza kulipa madeni hayo kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.

Wamesema hali hiyo imewaathiri kifedha kiasi kwamba imekuwa vigumu hata kukimu mahitaji ya familia zao.

“Tumekuwa watu wa kuomba omba na hakuna anayetilia maanani swala la malipo yetu yaliyosalia licha ya kukamilisha kazi,” amesema mmoja wao anayedai shilingi elfu 400.

Aidha wanakandarasi hao wamedai kuwa Wawakilishi Wadi katika kaunti hiyo wamekuwa kikwazo kwa biashara zao kwani wanashindana nao kupata zabuni zinazotolewa na serikali ya kaunti.

Wamelalamika kwamba Wawakilishi Wadi wanapewa kipaumbele wakati wa utoaji zabuni hizo.

Wanakandarasi hao ambao walikuwa wakizungumza mjini Kisumu wamewataka Wawakilishi Wadi hao kumakinika na kazi waliochaguliwa kutekeleza na kushinikiza serikali ya kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Anyang’ Nyong’o kushghulikia lalama zao na kuwalipa pesa zao.

Wamemtaka Gavana huyo kukabiliana na makundi ya walaghai ambao wamekuwa kizingiti kwao kupokea malipo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *