Wanahabari wa KBC Isaac Lemoka na  Lourdes Walusala watuzwa wanahabari bora

Wanahabari wa Shirika la Utangazaji la Kenya-KBC Isaac Lemoka na  Lourdes Walusala wametuzwa kwenye hafla ya kuwatunuku wanahabari bora  zaidi mwaka huu, kutokana na kazi yao ya kupigiwa mfano katika kuangazia athari za janga la Covid-19 hapa nchini.

Isaac Lemoka alitangazwa mshindi katika kitengo cha kuripoti kuhusu janga la Covid-19  huku Walusala akiibuka kuwa bora zaidi katika kitengo cha utayarishaji wa vipindi vya redio.

Isaac Lemoka alitayarisha makala kuhusu jinsi janga la Covid-19 lilivyoathiri hifadhi ya maziwa ya binadamu katika hospitali ya kujifungulia kina mama ya Pumwani na mikakati mbadala iliyowekwa ili kuhakikisha upatikanaji wa virutubishi maalum vya maziwa ya binadamu kwa watoto wachanga wakati wa janga hilo.

Kulingana na baraza la vyombo vya habari ambalo liliandaa hafla hiyo, lengo la tuzo hizo ni kuwatambua, kuwafurahia na kudumisha ubora wa wanahabari. Aidha Media Council of Kenya (MCK) inanuia kuwatambua wanahabari walioonyesha ubora wa hali ya juu katika taaluma yao, maadili yao kazini na kutambua ni vipi wanahabri wanavyoweza kupigwa jeki ili kudumisha viwango vya ubora katika taaluma yao.

Shughuli hiyo ya kuwatuza wanahabari iliyofanywa kupitia kwa njia ya video, iliongozwa na Kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Vyombo vya Habari hapa nchini Maina Muiruri na Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza hilo David Omwoyo.

Kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alidokeza kuwa wakati janga la Covid-19 lilipobisha hodi humu nchini na shughuli za kiuchumi kusitishwa, umuhimu wa vyombo vya habari kufahamisha umma yaliyojiri, ulikuwa wa kupigiwa mfano.

Kwa upande wake Omwoyo, alitaja kuwa licha ya chimbuko la vyanzo vya habari zisizo sahihi, wanahabari hapa nchini wameonyesha utaalam wa hali ya juu.

Kulingana na baraza la vyombo vya habari, kulikuwa na mawasilisho 1,119 lakini ni 18 tu walioibuka washindi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *