Wanafunzi wa shule za Kaunti ya Kitui kupokea barakoa bila malipo

Gavana wa Kaunti ya Kitui Charity Ngilu amesema kaunti hiyo inapanga kuanza kusambaza barakoa bila malipo katika shule za kaunti hiyo.

Akiongea katika kiwanda cha kushonea nguo cha Kitui KICOTEC alipokutana na maafisa wa elimu katika kaunti hiyo, Ngilu amesema kaunti hiyo mnamo itazindua usambazaji wa barakoa laki mbili kwa shule.

Amesema kaunti hiyo inatumia rasilimali zilizoko kusaidia shule ili kuweza kushughulikia wanafunzi wanaorejea shuleni baada ya kukaa nyumbani kwa muda wa miezi saba kutokana na chamko la ugonjwa wa COVID-19.

“Tutatumia rasilimali zilizopo kusaidia shule na barakoa, kemikali za kuua virusi na vifaa vya kupimia joto ili kuwezesha shule kurejelea masomo,” akasema.

Kulingana na Gavana Ngilu, serikali ya kaunti hiyo pia itatoa kemikali za kuua virusi zinazotengenezwa katika kaunti hiyo.

Amesema pesa zinazotolewa na serikali ya kitaifa ambazo ni shilingi 137 kwa kila mwanafunzi hazitoshi kuwezesha shule kumudu ununuzi wa barakoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *