Wanafunzi 52 wa shule ya upili ya wavulana ya Kolanya kaunti ya Busia waambukizwa Covid-19

Watu 60 wamethibitishwa kuambukizwa Covid-19 katika shule ya upili ya wavulana ya Kolanya,katika eneo bunge la Teso Kaskazini,kaunti ya Busia.

Visa hivyo vimetokana na sampuli 100 zilizopimwa. Kati ya watu hao sitini,52 ni wanafunzi ,walimu sita na wafanyakazi wawili.

Kufuatia tukio hilo,serikali ya kaunti ya Busia imewapeleka maafisa wa afya katika shule hiyo.

Kwenye kikao na wanahabari nje ya makao makuu ya serikali ya kaunti hiyo,Gavana wa kaunti hiyo Sospeter Ojaamong alisema waathiriwa wametengwa katika shule hiyo,ambapo wanashughulikiwa na maafisa wa afya.

Alisema wanafunzi wengine ambao hawakupatikana na virusi hivyo pia wamejitenga katika shule hiyo huku wakiendelea kuchunguzwa.

Gavana huyo amesema kaunti hiyo ni miongoni mwa zile ambazo zimeathirika zaidi tangu kubainishwa kwa kisa cha kwanza cha ugonjwa huo hapa nchini mwezi Machi mwaka huu.

Alisema kuna vituo viwili vya mpakani vya Busia na Malaba katika kaunti hiyo ambapo zaidi ya malori 1,500 ya mizigo hupitia kila siku na kuchangia ongezeko la maambukizi mapya katika kaunti hiyo .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *