Wana biashara wa Narok waomba serikali inusuru biashara zao zilizoathirika na janga la korona

Wafanyibiashara katika Kaunti ya Narok wanairai serikali ya kaunti hiyo kuwapunguzia ushuru ili kuzinusuru biashara zao kutokana na athari za janga la COVID-19.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama cha biashara na viwanda katika kaunti ya Narok David Mpatiany, biashara nyingi zinakumbwa na uhaba wa mtaji kufuatia kusitishwa kwa shughuli za usafiri katika kaunti tano zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa wa COVID-19.

Mpatiany alisema kupunguzwa kwa ushuru kutawasaidia wafanyibiashara kuanza upya baada ya kuathiriwa na janga hilo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Alitoa wito kwa gavana wa kaunti hiyo kupunguza ada za ardhi na leseni za biashara pamoja na ushuru wa maji na stima ili kuwakinga wakazi dhidi ya athari hizo.

Maoni yake yaliungwa mkono na mkurugenzi wa chama cha wafanyibiashara na viwanda katika kaunti hiyo Hezron Koori, aliyewahimiza wakazi kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya maambukizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *