Waliopewa zabuni za kuunda madawati ya shule watakiwa kuharakisha kazi hiyo

Waziri wa Elimu professor George Magoha amewahimiza wale waliopewa zabuni za kuwasilisha madawati kuharakisha shughuli hiyo ili kufanikisha kanuni ya kutokaribiana madarasani kuambatana na hatua za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Covid 19.

Akiwahutubia wanahabari katika kaunti ya Nandi baada ya kukutana na manaibu sita wa makamishna wa kaunti na wakurugenzi wa elimu, Prof. Magoha alisema kuwa pesa ziko za kugharamia utengenezaji wa madawati hayo.

Aliwahimiza maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa wanaoongoza kamati ya uundaji samani hizo kushirikiana na maafisa wa elimu na kuhakikisha kazi hiyo inakamilika.

Aliwataka maafisa hao kutayarisha hati zao vyema ili kuiwezesha wizara ya elimu kulipia madawati na mashubaka ambayo tayari yametengenezwa.  

Waziri huyo alielezea masikitiko kwamba ni asilimia 44 pekee ya madawati yaliyotengenezwa katika kaunti hiyo ilhali ina uwezo wa kuafikia asilimia 100.

Vile vile aliipongeza kaunti hiyo kutokana na juhudi zake za kuhakikisha kwamba wanafunzi wanarejea shuleni.

Na kuhusiana na swala la mimba za mapema, Prof. Magoha alikariri kwamba kila mtoto ni sharti arejee shuleni wakiwemo wasichana wajawazito.

Nandi ndio kaunti ya pili  bora zaidi baada ya Bomet katika kuhakikisha wanafunzi wanarejea shuleni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *