Waliopendekezwa kuwa mabalozi wasailiwa na kamati ya bunge

Watu watano waliopendekezwa na Rais  Uhuru Kenyatta kujaza nafasi za mabalozi 15, walisailiwa Ijumaa na kamati ya bunge la taifa kuhusu ulinzi na uhusiano wa kigeni.

Watu hao waliostaafu kutoka utumishi wa umma walitakiwa kuelezea ni kwa nini walikubali wito huo wa kurejea kazini.

Meja Jenerali mstaafu aliye na umri wa miaka 60 Ngewa Mukala ambaye alikuwa kamanda wa kikosi cha wana maji cha Kenya alitakiwa kuelezea kuhusu jinsi anavyonuia kuboresha uhusiano ya kibiashara kati ya Kenya na Sudan ambako atahudumu akiidhinishwa.

Wakili mkuu wa serikali katika wizara ya mashauri ya kigeni Stella Munyi, ambaye ananuia kuwakilisha nchi huko huko Zimbabwe alikabiliwa na wakati mgumu kuelezea kamati hiyo kuhusu utajiri wake wa shilingi milioni-91 ikizingatiwa mshahara wake wa kila mwezi.

Wengine waliosailiwa ni pamoja na balozi Jean Kimani aliyependekezwa kuwa balozi wa Kenya katika shirika la umoja wa mataifa kuhusu makazi jijini Nairobi na meja jenerali mstaafu Samuel Nandwa aliyependekezwa kuwa balozi wa Kenya nchini Sudan kusini.

Kamati hiyo ya bunge inayoongozwa na Katoo Ole Metito inatarajiwa kukamilisha shughuli ya kuwasaili waliopendekezwa kwenye nyadhifa za mabalozi Jumamosi kabla ya kuwasilisha ripoti yake bungeni.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *