Walimu waagizwa kurejea shuleni Jumatatu tarehe 28

Walimu wameagizwa kufika katika shule zao Jumatatu tarehe 28 katika kile kinachoonekana hatua ya kujiandaa kufunguliwa kwa shule hivi karibuni.

Hayo yametangazwa na afisa mkuu mtendaji wa tume ya kuwaajiri walimu nchini  Dr Nancy Macharia baada ya mkutano wa wadau katika sekta ya elimu ambao uliongozwa na waziri wa elimu Professor George Magoha.

“Tunawaagiza walimu kurejea shuleni Jumatatu tarehe 28 kujiandaa kwa ufunguzi wa shule. Walimu wetu wamejiandaa na wako tayari kuwasaidia wanafunzi kurejesha muda waliopoteza,” alisema Macharia.

Hata hivyo wizara ya elimu haijatangaza tarehe kamili ya kufunguliwa kwa shule.

Waziri wa elimu Prof George Magoha alisema tarahe ya kufunguliwa kwa shule itaamuliwa katika mkutano wa kiwango kingine.

Prof. Magoha aliwaruhusu wanafunzi wanaosomea shahada ya digrii katika maswala ya sayansi ambao walikuwa wakifanya mtihani wao wa mwisho kufanya mtihani huo kwa kuzingatia kikamilifu masharti makali yaliyowekwa na wizara ya afya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Waziri aliwahakikishia walimu walioajiriwa na bodi za usimamizi wa shule kuwa pesa zao zimetolewa na serikali huku akisisitiza kuwa watakaolipwa ni walimu walio na nambari za usajili za tume ya kuajiri walimu nchini-TSC.

Waziri aliwapuuzilia mbali wale wanaojaribu kuibuka na porojo za kuwepo kwa sakata katika mpango wa serikali wa kutoa shilingi bilioni 1.9 kwa mafundi wa  Jua kali kutengeneza madawati na viti kwa shule huku akisisitiza kuwa pesa hizo hazitafujwa au kuibwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *