Wakulima wa Samburu kunufaika na tawi jipya la shirika la utoaji mikopo la AFC

Shirika la utoaji mikopo kwa sekta ya kilimo, (AFC) limefungua upya tawi lake la kaunti ya Samburu ambalo lilifungwa miaka 20 iliyopita.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tawi hilo mjini Maralal, kaimu mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Rose Ochanda alisema tawi hilo lilifungwa mwaka 1996 baada ya kuhudumu kwa miaka 9 pekee kutokana na changamoto za kifedha.

Kulingana na Ochanda shirika hilo litashirikiana kwa karibu na serikali ya kaunti ya Samburu ili kuboresha shughuli za kilimo kupitia kuwapa wakulima mikopo nafuu.

“Kaunti ya Samburu ina uwezo mkubwa sana wa ustawishaji kilimo huku eneo lake likiwa kilomita 1,580 mraba,” alisema Ochanda.

Kwa upande wake mwenyekiti wa shirika hilo la AFC, Franklin Bett aliwahimiza wakazi wa Samburu wasiuze mashamba yao ila wachukue mikopo ya kuimarisha uzalishaji maziwa na kilimo cha mimea.

“Kutoa uhamasisho kwa wakazi wa eneo hili kuhusu manufaa ya AFC litakuwa lengo kuu la afisi hii ya Maralal. Wamiliki mashamba wanaweza kutumia hatimiliki ya mashamba kuchukua mikopo nafuu,”alisema Bett.

Wakati uo huo Bett alielezea umuhimu wa kulipa mikopo akisema enzi za wanasiasa kufutilia mbali madeni imepitwa na wakati.

“Ikiwa mtu anachangamoto ya kulipa deni lake, afisi zetu ziko wazi kwa mashauriano,” alisema Bett.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *