Wakulima wa miwa wapinga ukodishaji viwanda vya sukari
Wakulima wa miwa katika kaunti ya Nandi wamepinga uamuzi wa serikali wa kukodisha viwanda vya sukari.
Wakulima hao kwa ushirikiano na Gavana wa Nandi, Stephen Sang, sasa wanamtaka waziri wa kilimo Peter Munya, abatilishe uamuzi huo na kuruhusu ushiriki wa umma.
Gavana Sang alisema kwamba waziri huyo alipaswa kufanya maamuzi kulingana na ripoti ya jopo lililobuniwa 2018, kujadili maswala yanayoathiri sekta ya sukari nchini, na ambalo lilipendekeza ubinafsishaji wa viwanda na wala sio kukodishwa viwanda.
“ Tulikutana na jopokazi na kujadiliana na wadau pamoja na wakulima kisha tukakubaliana viwanda hivyo vibinafsishwe,” alisema Sang
Katibu wa chama cha wakulima wa miwa katika kaunti ya Nandi, David Sum, alikosoa hatua ya waziri wa kilimo ya kukodisha kampuni za sukari bila hata kutangaza hadharani sheria na masharti ya makubaliano ya kukodishwa kwa viwanda hivyo.
“ kama wakulima wa miwa, tulienda mahakamani kuzuia hatua ya waziri wa kilimo na mahakama ilisitisha hatua hiyo hadi kesi iliyowasilishwa itakapoamuliwa,” alisema Sum.
Kaunti hiyo ina zaidi ya wakulima elfu 20 ambao ni sehemu ya wakulima wa miwa wa kanda ya Nyando.
Viwanda vinavyotarajiwa kukodishwa ni Chemelil, Miwani, Sony na Nzoia, kwa kipindi cha miaka 25.