Wakenya wahimizwa kujibu arafa za kuchukua kadi ya huduma namba

Wakenya wamehimizwa kujibu jumbe wanazotumiwa za kuwataka kuelezea mahali ambako wangependa kuchukua kadi zao za Huduma.

Kwa mujibu wa msaidizi wa kamishna wa kaunti, Spinica Makori ambaye anaongoza kundi linalohusika na utoaji mafunzo, Wakenya wameanza kupata arafa kuhusu Huduma Namba na kwamba shughuli hiyo itaendelea hadi mwezi Disemba mwaka huu.

Akiongea Ijumaa wakati wa warsha ya siku mbili ya kutoa mafunzo kwa makarani wa kutoa Kadi za Huduma,  Makori alisema Wakenya wamekuwa na mazoea ya kusubiri hadi siku za mwisho mwisho wakati wa shughuli za kitaifa kama hiyo.

Kwa kuwa sasa tumezindua rasmi zoezi hilo kote nchini na tumewafunza maafisa wetu ambao wataendesha zoezi hilo la kuwapa wakenya kadi hizo, kitakachofuata sasa ni ujumbe mfupi kwa simu zenu, tunawasihi kuitikia ujumbe huo,” alisema Makori.

Aidha, alitoa wito kwa makarani hao kumakinikia kazi yao ya kutoa kadi za Huduma ambazo zina maelezo ya siri.

Kamishna wa kaunti ya Garissa, Meru Mwangi pia amewahimiza wakenya na maafisa wa usajili kumakinikia shughuli hiyo inayolenga kupunguza kadi ambazo Wakenya wanahitajika kuwa nazo.

Mnamo mwaka-2015, serikali ilizindua shughuli ya kusajili Wakenya kielektroniki kupitia mfumo wa pamoja wa usajili wa watu kidijitali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *