Wakazi wa Pokot Magharibi wanufaika na barakoa kutoka ubalozi wa Marekani nchini

Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umetoa mchango wa barakoa elfu-100 kwa kaunti ya Pokot Magharibi kama sehemu ya juhudi zake za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Barakoa hizo zitasambaziwa watoto wa shule katika eneo hilo.

Akiongea huko Kapenguria wakati wa kuwasilisha barakoa hizo balozi wa Marekani nchini Kenya Kyle McCarter alisema uhusiano wa kirafiki ulioko baina ya Kenya na Marekani ungali imara.

Balozi huyo aliongeza kuwa barakoa hizo zenye maandishi ya “USA Marafiki” ni mradi unaodhamiria kuhakikisha kwamba watoto wanarudi shuleni wakiwa salama.

Wakati huo huo balozi huyo alitembelea miradi miwili inayofadhiliwa na ubalozi wa Marekani, na kuwataka wakaazi waanzishe miradi ya kuwaletea mapato.

Kundi la kujisadia la kina mama la “Ewan Kiror” ambalo lilinufaika na chumba cha kuwawezesha kukuza Pili Pili ndani ya ukumbi liliomba usaidizi zaidi ili kujenga kumbi nyingine za kukuza mazao mbali mbali kama vile nyanya.

Mwenyekiti wa kundi la kina mama la Otupo katika eneo la Kapkoris- Elizabeth Keriso, aliitisha ufadhili zaidi ili wajihusisha na mradi wa ufugaji kuku na kufaidi wanachama wengi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *