Wakazi wa Kisiwa cha Faza, Lamu walalamikia kuchelewa kwa mradi wa maji

Wakazi wa Kisiwa cha Faza, Kaunti ya Lamu wanaiomba serikali ya kaunti hiyo kukamilisha upesi mradi kutoka Vumbe kuelekea Faza.

Wakazi hao wanalalamikia kuchelewa katika utekelezwaji wa mradi huo wakidai kuwa ulizinduliwa miaka kadhaa iliyopita na tayari mamilioni ya pesa yalitumika.

Baadhi yao walizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa maji kidogo yanayopatikana katika kisiwa hicho yana chumvi nyingi kiasi cha kutoweza kusaidia katika matumizi ya nyumbani.

Wamesema wanategemea maji ya mvua kwa kuwa hakuna maji safi ya mfereji yanayofika katika kisiwa hicho na kulaumu uongozi wa serikali ya kaunti kwa kutowajibika kuukamilisha mradi huo.

“Twaiomba serikali ya kaunti iharakishe ukamilishaji wa mradi huu ili tupate maji safi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani,” akasema mmoja wa wakazi hao.

Wakazi hao wamesema mradi huo utawapa afueni kwani sasa wanalazimika kununua maji kutoka sehemu zengine kwa bei ghali.

Wakati wa kiangazi, wakazi hao hutumia hadi shilingi 250 kwa kila mtungi wa lita 20 za maji.

“Tumekuwa tukitoa maji kutoka eneo la Tchundwa na baadaye tukawa na tumaini kwamba mradi huu wa kuleta maji ya mfereji utatusaidia lakini sasa tunahofu kwamba huenda jambo hili lisitimie.”

Juhudi za kupata taarifa kutoka kwa Idara ya Maji ya serikali hiyo ziligonga mwamba baada ya Mkuu wa Idara hiyo Paul Kimani kusema kuwa ako hospitalini na angewasiliana na waandishi wa habari baadaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *